Jumatano , 3rd Feb , 2021

Mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania Adi Yussuf amesajiliwa na klabu ya soka ya  Chesterfield inayoshiriki ligi ya Taifa maarufu kama 'Vanarama National league', ambayo ni daraja la tano kwa ukubwa kutokana na mfumo wa soka  England.

Adi Yussuf (kulia) akiwa na nahodha wa timu ya Tanzania Mbwana Sammata katika mazoezi ya timu ya Taifa

Yussuf anasajiliwa akitokea klabu ya Wrexham aliyokuwa anatumikia kwa mkopo lakini usajili wake wa kudumu upo Blackpool.

''Nina furaha kubwa kujiunga na timu hii, binafsi ninaiheshimu ni kubwa na ni nzuri katika maisha yangu ya soka, nawafahamu baadhi ya wachezaji na mambo ya klabu kiujumla naamini nitafanikiwa nikiwa hapa'' alisema Yussuf.

Adi Yussuf ni Mtanzania aliyezaliwa Zanzibar mwaka 1992 na kisha kukulia England alianza kucheza soka mwaka 2011 katika klabu ya Leicester City, inayoshiriki ligi kuu kwa sasa, ni mabingwa wa mwaka 2015 /2016 , aliondoka katika timu hiyo baada ya mkataba wake kuisha.

Yussuf ni mchezaji wa zamani wa Taifa Stars aliyeshiriki katika michuano ya AFCON mwaka 2019 nchini Misri, aliitwa kwa mara ya kwanza katika timu ya Taifa mwaka 2015, lakini hakupata nafasi ya kucheza hata mchezo mmoja.

Mshambuliaji huyo ambaye alisababisha Shirikisho la soka TFF kupigiwa kelele kwa kutomjumuisha mara kwa mara kwenye kikosi cha Taifa stars, kwa mara ya kwanza alicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Zimbabwe juni 16 2019 Cairo Misri kabla ya kucheza mchezo wa kimashindano katiaka AFCON dhidi ya Algeria.